Wednesday, August 10, 2016

    Dady

    Kilimo Bora Cha Migomba

    UTUNZAJI WA SHAMBA NA MIMEA.

    (a) Uwekaji wa matandazwa
    Kazi hii ni vyema ikafanywa mara baada ya kupanda kama inawezekana.
    Matandazo yawe ni makavu na unene wa sentimeta 15 ili kuhifadhi
    unyevu, kuzuia magugu na yakioza yataongeza mbolea.

    (b) Uongezaji wa mbolea
    Baada kupanda ni vyema kuongeza mbolea madebe 2 kuzunguuka shina
    la migomba kila baada ya miaka miwili au mitatu. Mbolea hii inatakiwa
    kuchanganywa na udongo na kufunikwa kwa matandazwa.

    (c) Umwagiliaji maji shambani
    Migomba huhitaji maji mengi. Wakati wa kiangazi. Inafaa kumwagilia ili
    kuto kupunguza sana ukubwa na wingi wa ndizi zinazotarajiwa kuvunwa
    kwa mwaka. Kiasi cha maji kinachotakiwa kwa wiki ni milimita 25,
    yaani eneo linalo zunguka shina la migomba lilowe kabisa.
    (d) Kupunguzia machipukizi
    Inatakiwa kupunguza mimea ya migomba kwa kila shina na kubaki
    mimea mitatu tu, yaani Mgomba wenye ndizi (Mama), Mgomba
    mkubwa ambao bado haujazaa lakini unakaribia kuchanua (Mtoto),
    Mgomba mchanga uliochipua hivi karibuni ( Mjukuu)
    (e) Uondoaji wa Majani Makavu
    Mimea ya migomba inafaa iondolewe majani yote makavu ili kuondoa
    uwezekano wa kuwepo mazalia ya wadudu na magonjwa, kuruhusu
    mionzi ya jua na kufanya urahisi wa kuhudumia shamba .Pia hufanya
    shamba kuonekana safi.
    (f) Uondoaji wa ncha mwishoni mwa matunda
    Baada ya mkungu kutoa ndizi, ua hunyauka na kubakiza ncha mwishoni
    mwa matunda. Ncha hizo hupaswa kuondolewa .Huduma hii husaidia
    kupunguza uwezekano wa kujeruhi matunda wakati wa kusafirisha
    jambo ambalo kupunguza ubora wa tunda.
    (g) Kuweka Miega
    Miega ni nguzo au kamba ambazo hutumika kuzuia migomba iliyobeba
    mikungu mikubwa isianguke kutokana na uzito mkubwa. Miega ni ya
    lazima katika sehemu zenye upepo mkali. Kazi hii inatakiwa kufanywa
    kwa uangalifu ili isijeruhi ndizi na mgomba wenyewe.
    (h) Uondoaji wa kichombezo cha ua la kiume (Shumba)
    Uondoaji wa shumba huwezesha matunda kukua vizuri, kuongezeka
    uzito wa mkungu pia huzuia magonjwa kama vile ugonjwa wa mnyauko
    wa migomba (Banana Baterial Wilt), ugonjwa wa Majivu nchani mwa
    matunda (Cigar end rot). Ukataji hufanyika juu ya kovu la pili baada ya
    kichana cha mwisho, kwa kutumia kisu kikali.
    UVUNAJI
    Zao la ndizi huweza kuanza kuvunwa katika kipindi cha miezi 9 hadi
    miezi 15 tangu kupandwa kwa chipukizi. Muda wa kuvunwa hutegemea
    hali ya hewa. Katika sehemu za joto ndizi huvunwa mapema zaidi kuliko
    sehemu za baridi. Pia migomba iliyopandwa kwa kutumia machipukizi
    huzaa mapema kuliko iliyopandwa miche iliyozalishwa kwa chupa
    (tissue culture)

    MATUMIZI YA RIBONI
    Riboni za rangi moja (au alama ya kamba) hufungwa kwenye migomba
    ya umri mmoja mara tu inapoanza kuchanua, na riboni ya rangi nyingine
    hufungwa kwenye migomba itakayoanza kuchanua wiki mbili hivi
    zinazofuata na kuendelea hivyo ili kurahisisha kuitambulisha mikungu
    ambayo itavunwa kwa wakati mmoja. Pia matumizi ya riboni hurahisiha utunzaji wa kumbukumbu ili kujua ni lini na ni mikungu mingapi itavunwa.

    WAKATI UNAOFAA KUVUNA
    Mkungu wa ndizi huweza kuvunwa katika hatua tofauti kulingana na matumizi, aina na mahitaji ya soko. Mkungu huachwa kwenye mgomba mpaka vidole (matunda ) vimejaa. Uzito wa mkungu hongezeka haraka
    katika wiki mbili za mwisho, ambapo migongo ya ndizi hutoweka.
    Ndizi zinaweza kuvunwa zikiwa zimekomaa na zimeiva kwa kiasi cha asilimia 75 kwa ajili ya kusafirishwa mbali, pia zinaweza kuvunwa zikiwa kukomaa na zimeanza kuiva kwa ajili ya soko la karibu, au zikiwa
    zimekomaa na kuiva kabisa kwa ajili ya soko na matumizi ya nyumbani
    Njia bora ya kukata mkungu, ni ile inayohakikisha kuwa mkungu wa ndizi hauanguki chini na kuvunja, kuchubuan au kuharibu ndizi, jambo ambalo litapunguza ubora. Ukichelewa kuvuna ndizi zinaweza kuharibiwa na ndege, wanyama, wadudu au kuibiwa.

    UBORA WA NDIZI
    Ndizi zenye sifa nzuri sokoni ni zile ambazo zimekomaa kwa kiasi
    kinachotakiwa na zenye vidole vyenye urefu mzuri na visivyo na
    michubuko. Pia ziwe hazijashambuliwa na magonjwa wala wadudu
    waharibifu.

    KIASI CHA MAVUNO
    Mavuno ya ndizi hutegemea zaidi aina ya migomba, hali ya hewa, utunzaji wa mimea shambani. Mavuno huweza kufikia hadi tani 60 au zaidi kwa hekta kwa mwaka. Hata hivyo mavuno mazuri kwa mkulima
    wa kawaida yasipungue kati ya tani 20 hadi 30 kwa hekta kwa mwaka.

    MAGONJWA
    Ugonjwa wa hatari sana ulioingia hivi karibuni katika wilaya ya Muleba
    na maeneo mengine mkoani Kagera kutoka nchi jirani ya Uganda ni wa
    Mnyauko wa migomba unaosababishwa na bakteria (Banana Bacterial
    Wilt). Magonjwa mengine yanayosumbua zao hili ni Kuoza tunguu,
    Ugonjwa wa panama, Ugonjwa wa majivu nchani mwa tunda, Sigatoka,
    na Moko.

    WADUDU WAHARIBIFU
    Wadudu wanaosumbua zaidi hili ni Minyoo fundo (Banana nematodes),
    na Vifukuzi (Banana weevils).

    UDHIBITI WA MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU
    Magonjwa na wadudu hawa huweza kuepukwa kwa kufuata kanuni bora
    za uzalishaji wa zao hili. kama usafi wa shamba na kuchagua chipukizi
    bora. Au kupanda miche iliyozalishwa kwa chupa (Tissue culture banana
    seedlings) Hata hivyo mara mataizo haya yakitokea muone mtaalam wa
    kilimo aliye karibu ili aweze kukupa ushauri.

    • Dalili za ugonjwa wa mnyauko wa migomba unaosababishwa na bakteria